KAMATI ya Maadili ya wabunge imemaliza kuwahoji wabunge watatu Josephat Gwajima Mbunge wa Jimbo la Kawe, Jerry Silaa Mbunge wa Jimbo la Ukonga na Mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole.

Akiongea mara baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo Hassan Mtenga Mwenyekiti wa Kamati ya maadili na pia  Mbunge wa Mtwara mjini amesema wameanza kikao hicho mnamo majira ya saa 2 asubuhi ambapo kamati hiyo imewasikiliza na kuwahoji wabunge hao.

" Tumewasikiliza kama kamati na sisi pia tutakwenda kuwasilisha taarifa za  mahojiano haya kwenye kamati ya uongozi wa bunge ambayo mwenyekiti wake ni Kasim Majaliwa mbunge wa jimbo la Ruangwa," amesema  Mtenga

Mahojiano hayo yalianza majira ya saa 2 asubuhi ambapo wakwanza kuhojiwa alikuwa ni Humphrey Polepole aliyewasili mapema katika viwanja vya CCM makao makuu.

Wa pili kuhojiwa na Kamati hiyo alikuwa ni mbunge wa Jimbo la Ukonga ambapo aliwasili na kwenda kuhojiwa majira ya saa 5 na Nusu asubuhi na kutoka majira ya 6 :27 mchana

Na wa mwisho kuhojiwa alikuwa mbunge wa Kawe Josephat Gwajima ambae alihojiwa kwa muda wa masaa matatu kuanzia saa 6:28 mchana na hadi saa 8 na Dakika 20 mchana.