SERIKALI imesitisha bei mpya ya mafuta ya petroli na dizeli iliyotangazwa  hivi karibuni na Mamlaka ya Mafuta na Maji (EWURA) ambazo zilitarajiwa kuanza Septemba 1 mwaka huu na kuagiza tume ifanye uchunguzi kuhusu bei hizo.

 

Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Septemba 4, 2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na wanahabari jijini Dodoma na kuongeza kuwa bei ya zamani itaendelea.

 

“Kulitokea taarifa mbili, kwanza EWURA walitoa bei mpya za mafuta kuanzia Septemba 1, baadaye wakasitisha. Waziri Mkuu aliliona hilo akaagiza bei hizo mpya ziangaliwe upya, lakini bei za awali zinaendelea. Kwa hiyo sasa hivi zinaendelea bei za mwezi Agosti.

 

“Kamati aliyoagiza Waziri Mkuu kuchunguza suala la bei ya mafuta tayari imeanza kazi, itatoa ripoti baada ya wiki mbili. Wataangalia mfumo wa ukokotoaji wa bei, utaratibu wa ununuzi wa mafuta, tozo, kampuni zinazoagiza mafuta nje na utaratibu uliowekwa bandarini.

 

“Lengo ni kujua sababu za kupanda kwa mafuta na kujua kama kuna maeneo yanayoweza kushughulikiwa ili Watanzania waendelee kupata mafuta kwa bei nafuu, kwani kupanda kwa bei ya mafuta kuna madhara katika uchumi,” -Gerson Msigwa.