WAJASIRIAMALI RUVUMA WATAKIWA KUTUMIA VIPATO VYAO NA FAMILIA ZAO.

Katibu tawala msaidizi wa mkoa wa Ruvuma Bakari Mketo mwenye suti ya blue akiangalia bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa mkoa huo.


Na Amon Mtega, Ruvuma.

WANAWAKE Wajasiriamali Mkoani Ruvuma wametakiwa kutumia vema vipato vyao vinavyotokana na ujasiriamali huo ,kwa kusaidia familia zao na kuachana na tabia ya kuwa chanzo cha kuzigawa familia.

Wito huo umetolewa na  katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma Bakari Mketo wakati akizindua maonyesho ya siku saba ya bidhaa zinazozalishwa na wanawake wa mkoa huo(Tanzania Women Chamber of Commerce).


Mketo ambaye amekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wakinamama wajasiliamali kutumia vipato vyao kuzinyanyasa familia wakiwemo na waume zao jambo ambalo hupelekea familia hizo kuvurugana.

Aidha katibu Tawala msaidizi huyo amesema kama wakinamama hao watatumia vipato vyao vema kwa kushirikisha familia zao basi familia nyingi zitajikwamua kiuchumi ikiwemo watoto wao kupatiwa elimu.

Hata hivyo amewapongeza wanawake hao kwa ujasiriamali wanaoufanya huku akiwataka baadhi yao kwenda kuzisajili bidhaa zao ili kukidhi ushindani wa kibiashara ambao wengi wao wamekuwa wakishindwa kutokana na bidhaa zao kutokuzisajili .

Amesema kuwa Serikali imeshaweka mifumo mizuri ya kuyakwamua kiuchumi makundi mbalimbali kwenye jamii ikiwemo wanawake kwa kupitia mikopo kwenye taasisi za kibenki pamoja na fedha za asilimia kumi ambazo hutolewa na Halmashauri.

Mwenyekiti wa wanawake wa mkoa wa Ruvuma Rosemary Ngonyani akizungumzia juu ya uwajibikaji wa wanawake hao kwenye ujasiliamali.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Wanawake mkoa wa Ruvuma Rosemary Ngonyani  awali akisoma risala kwa mgeni rasmi huyo amesema wanawake hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosa masoko ya uhakika ya kuuzia bidhaa zao.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa licha ya changamoto ya masoko lakini hadi sasa idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia 120 kutoka katika Wilaya zote za mkoani humo.

Afisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri Mbinga Vijijini Huruma Komba akizungumzia ufanyaji kazi wa vikundi vitatu  anavyovisimamia ambavyo vimekuwa moja ya vikundi vya mfano katika Halmashauri hiyo.

Naye mmoja wa washiriki Huruma Komba amesema kuwa yeye anasimamia vikundi vitatu vya kutoka katika Halmashauri ya Mbinga Vijijini vimekuwa vikifanya vizuri lakini kufuatia maonyesho hayo vitafanya vizuri zaidi.

Komba ambaye ni afisa maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Mbinga Vijijini amevitaja vikundi hivyo ni Tuinuane mpapa ambacho hutengeneza mvinyo,Mkombozi group ambacho hutengeneza taulo za kike na Innovation group ambacho hutengeneza Sabuni.

Post a Comment

0 Comments