Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Joseph Konyo akizungumza na madereva wa Serikali wa Mkoani humo wakati akifungua mafunzo ya kujikumbusha kuhusu masuala ya usalama barabarani.

NA AMON MTEGA,RUVUMA.

KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Joseph Konyo amewataka madereva wa Mkoa huo wanaoendesha vyombo vya moto vya Serikali(UMMA) kuwa mfano bora kwa madereva wengine ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikitokea ambapo baadhi ya ajali zimekuwa zikisababishwa na madereva wa Umma.

Wito huo ameutoa wakati akifungua mafunzo ya kukumbushana kuhusu wajibu wa madereva hasa waserikali wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto ikiwemo magari kuzingatia alama za barabarani ambayo yamefanyika katika ukumbi wa ofisi za usalama barabarani zilizopo Msamala.

Kamanda Konyo akizungumza na madereva wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Jeshi la Wananchi Tanzania amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya madereva wa Serikali kupuuzia alama za barabarani na kupelekea kusababisha ajali jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na Wananchi wakiwemo madereva wasio wa Umma.

Amesema kuwa inashangaza kuona dereva wa Serikali sehemu ya makazi ya watu anaendesha kwa kasi ambayo haikubaliki na pia sehemu za waenda kwa miguu (Zebra)madereva wamekuwa hawasimami ili kumruhusu mwenda kwa miguu kuvuka.

Hata hivyo amesema kuwa kuanzia sasa baada ya kupeana mafunzo ya kukumbushana kuhusu wajibu wa dereva awapo barabarani amewataka wakabadilike ili wakawe mfano bora kwa madereva wengine .

Kamanda wa usalama barabarani Mkoa wa Ruvuma Salumu Morimori akiwaambia madereva wa Serikali wa mkoa huo kuwa atakayekiuka sheria za barabarani kuchukuliwa hatua bila kujali kama ni dereva wa Serikali.

Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha usalama barabarani wa mkoa wa Ruvuma Salumu Morimori amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya madereva hao kuwadharau hata askari wa usalama barabarani pindi wanaposimamishwa ili wapewe taratibu ya kuchukua tahadhari jambo ambalo amesema halitakiwi.

Morimori amesema kuwa askari wa usalama barabarani anapokuwa anamsimamisha dereva wakati akiendesha chombo cha moto asichukuliwe kama anachelewesha safari bali achukuliwe kuwa anataka asaidie mfike salama kwenye safari yenu .

“Baadhi yenu madereva wa Serikali mnajisahau na kujifanya mpo juu ya sheria nawaambieni hakuna mtu ambaye anakuwa juu ya sheria ukikosea utawajibishwa ipasavyo”amesema Salumu Morimori kamanda wa usalama barabarani.

Mmoja wa madereva wa Serikali mkoa wa Ruvuma Jiofrey Claudius akipongeza mafunzo hayo na kuwa yamewasaidia kuwakumbusha.

Naye mmoja wa madereva hao Jofrey Craudius amesema kuwa anashukuru kwa mafunzo hayo ya kukumbushana wajibu na kuwa jamii hasa kwa madereva wasiyo wa Serikali wategemee kuona mabadiliko ambayo yatakayo wafanya waige mfano wawapo kwenye vyombo vya moto.