Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde akitangaza matokeo hayo jana Oktoba 30 jijini Dar es Salaam amesema watahiniwa 1,108,023 sawa na asilimia 97.87 ya waliosajiliwa walifanya mtihani huo.
Watahiniwa 907,820 kati ya 1,107,460 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 81.97.
Dk Msonde amesema Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na shule 715 na watahiniwa 81,562 walishiriki mtihani huo ambapo waliofaulu ni 78,738 sawa na asilimia 97 ya watahiniwa wote katika mkoa huo.
Kwa ufaulu huo wa Dar es Salaam umeufanya mkoa huo kuongoza kitaifa ukifuatiwa na Iringa ambapo ufaulu wake ni asilimia 91 ya wanafunzi 28,018 waliofanya mtihani.
Mbeya imeshika nafasi ya tatu ambapo asilimia 88 ya watahiniwa 44,822 waliofanya mtihani huo wamefaulu ikifuatiwa na Arusha katika nafasi ya nne.
Nafasi ya tano imeenda kwa Mkoa wa Njombe.Njombe ilikuwa na watahiniwa 20,314 lakini waliofaulu ni 17,652 sawa na asilimia 86.9 ya watahiniwa wote katika mkoa huo.
Kilimanjaro imeshika nafasi ya sita ikifuatiwa na Mkoa wa Katavi katika nafasi ya saba kwa wanafunzi wake kufaulu kwa asilimia 87 sawa sawa na Kilimanjaro.
Wakati Katavi ikishika nafasi ya saba, katika orodha hiyo, Lindi iko nafasi ya nane ikifuatiwa na Simiyu ambayo imeshika nafasi ya tisa.
10 bora imefungwa na Mkoa wa Pwani ambapo wanafunzi 32,331 kati ya 38,079 sawa na asilimia 85 katika mkoa huo wa mashariki mwaka Tanzania wamefaulu mtihani huo uliofanyika Septemba 8 na 9 mwaka huu.
0 Comments