Na.Amon Mtega,SONGEA.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amemuonya mfanyabiashara Tito Mbilinyi (MWILAMBA) wa Manispaa ya Songea Mkoani humo kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kwa maslahi ya jamii na siyo maslahi ya mtu binafsi.
Wito huo ameutoa kufuatia kuibuka kwa sakata la huduma ya choo kilicho fungwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (SOUWASA) kwaajili ya kupisha ujenzi wa mradi wa tenki la maji ya bomba ambao utasaidia kupunguza adhaa ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.
Ibuge akizungumzia sakata hilo ambalo liliibuliwa na mfanyabiashara huyo kuhusu kufungwa kwa choo hicho wakati wa kikao cha dharura cha kujadili namna ya utoaji wa elimu kwenye jamii juu kupatiwa chanjo ya UVIKO 19 amesema kuwa ni vema tukajadili maslai ya wananchi na siyo maslai yetu.
Mkuu huyo ambaye alianza kwa kusikiliza sakata hilo kwa pande zote zenye mamlaka juu ya suala hilo amesema kuwa mfanyabiashara huyo anatakiwa kufuata taratibu za kisheria kwa mujibu wa kanuni zilizopo licha ya kuwa jambo hilo lipo mahakamani.
“Nakuomba Bw, Tito Mbilinyi(MWILAMBA) tunapokuwa kwenye vikao kama hivi tuache kujadili maslai yetu binafsi bali tujadili maslahi ya wananchi wetu hasa katika kupambana na janga hilo la ugonjwa wa Corona na jambo hilo tayari lipo mahakamani hivyo tusilijadili sana tuiachie mahakama”amesema Ibuge.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani humo Pololeti Mgema alipoambiwa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma atolee ufafanuzi juu ya sakata hilo kwenye kikao hicho amesema kuwa hakuna sababu ya kujadili sana kwa huduma ya choo hicho kwa kuwa ilikuwa ni biashara ya mtu binafsi ambaye ni Tito Mbilinyi na kuwa aliweka huduma hiyo kwenye eneo la SOUWASA ambapo wanahitaji kujenga tenki kubwa la maji kwa matumizi ya wananchi.
Mgema ameongeza kusema kuwa jambo hilo lipo mahakamani na kuwa jambo lolote likiwa mahakamani halihitaji kujadiliwa sana ila kwa kuwa yeye kaamua kulileta kwenye kikao hiki basi imetupasa tutolee ufafanuzi .
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Philipo Beno akitolea ufafanuzi kuhusiana na sakata la choo kilichokuwa kikimilikiwa na mfanyabiashara Tito Mbilinyi(MWILAMBA). |
Naye kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Philipo Beno amesema kuwa katika eneo la stendi ya daladala iliyopo Mfaranyaki hakuna tatizo la vyoo vya abiria na vipo vya kutosha na kuwa choo kinacholalamikiwa na mfanyabiashara huyo kilikuwa nje ya stendi hiyo na kuwa ndiye mmiliki .
Kaimu mkurugenzi huyo amesema kuwa hata ufungaji wa vyoo hivyo wamefunga watu wa SOUWASA na kuwa eneo hilo ni rasmi kwaajili ya mradi wa ujenzi wa Tenki la maji.
Mfanyabiashara Tito Mbilinyi (MWILAMBA) akizungumzia kufungwa kwa choo alichokuwa akimiliki yeye ambacho kinadaiwa kipo kwenye eneo la SOUWASA. |
Mfanyabiashara Tito Mbilinyi alinyoosha kidole kwenye kikao hicho na kuruhusiwa na mwenyekiti wa kikao ambaye ni mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akasema kuna choo kimefungwa eneo la stendi ya daladala Mfaranyaki na kusababisha watu kushindwa mahali kwa kujisaidia jambo ambalo hupelekea msongamano unaoweza kusababisha milipuko ya magonjwa ikiwemo Corona.
Mbilinyi hakutaka kuweka wazi nani mmiliki halisi wa choo hicho hadi pale mwenyekiti wa kikao alipopata ufafanuzi kutoka kwa wasaidizi wake ambao ni mkuu wa Wilaya ya Songea Pololeti Mgema pamoja na kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Philipo Beno na kisha kubaini kuwa mmiliki ni mfanyabiashara huyo.
0 Comments