KATIKA kuuaga mwaka 2021 kisha kuukaribisha mwaka 2022 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Ruvuma limeishukuru kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa kuwasaidia kukarabati gari la kufanyia shughuli za zimamoto ambalo ukarabati wake umetumia zaidi ya Sh.Milioni tatu ( 3,000,000).
Akitoa shukrani hizo ambazo zimeenda sambamba na kutakiana heri ya kuukaribisha mwaka 2022 kamanda wa Zimamoto Mkoani Ruvuma mlakibu msaidizi Salehe Mkegeto amesema kuwa utengenezaji wa gari utalisaidia jeshi hilo kufanya kazi ya uokoaji pindi matukio yanapokuwa yamejitokeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye jamii.
Kamanda Mkegeto amesema gari hilo lilikuwa bovu hasa kwenye bodi ambalo lilikuwa likivujisha maji kiasi kwamba yalikuwa hayawezi kufika eneo la tukio jambo ambalo lilikuwa likiwasababishia kukwamisha shughuli za uokoaji.
Meneja wa Uhusiano wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited Khadija Pallangyo akimkabidhi ufunguo wa gari kwa kamanda wa kikosi cha Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Ruvuma ,Salehe Mkegeto. |
Hata hivyo licha ya kutoa shukrani hizo kwenye kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayojishughulisha na madini ya Uranium katika mto Mkuju uliopo Wilaya ya Namtumbo Mkoani humo kamanda huyo amewaomba wadau wengine waweze kujitokeza kusaidia kukarabati vitendea kazi vya kikosi hicho likiwemo gari lililopo Wilaya ya Mbinga ambalo limekuwa chakavu linahitaji msaada wa matengenezo.
Afisa habari wa Kikosi cha Zimamoto na uokoaji Mkoani Ruvuma,Annastazia Fasha akizungumzia changamoto ya uhaba wa vitendea kazi vya Zimamoto hilo. |
Naye upande wake Annastazia Fasha ambaye ni afisa habari wa kikosi hicho amesema kuwa jeshi limekuwa likikabiliwa na changamoto ya vitendea kazi hivyo kampuni ya Mantra Tanzania Limited imeonyesha njia kwa wadau wengine wajitokeze ili kuimarisha kikosi hicho kwa kuwa na vitendea kazi vya uhakika.
Naye meneja mahusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Limited,Khadija Pallagyo amesema kuwa kampuni hiyo imeamua kutoa msaada wa kulikarabati gari hilo baada ya kutambua kazi kubwa inayofanywa na Jeshi hilo katika kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo ya moto.
Meneja mahusiano huyo amesema kuwa licha ya Jeshi hilo kufanya kazi ya uokoaji lakini pia limekuwa likipita kutoa elimu ya kujikinga na majanga yakiwemo ya moto ambapo hadi kwenye maeneo yanakotakiwa kuchimbwa Urani wameenda kutoa elimu ambapo ni umbali wa zaidi ya klometa 140 kutoka Songea mjini .
Kampuni ya Mantra mara kwa mara imekuwa ikishirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali .
0 Comments