MADEREVA WA VYOMBO VYA MOTO RUVUMA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI.



NA AMON MTEGA, SONGEA.

MKUU wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoani Ruvuma mrakibu wa Polisi Salum Morimori amewataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia kanuni za udereva ili kuepusha ajali ambazo hutokea kutokana na uzembe.


Wito huo ameutoa wakati alipofanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye vituo vya mabasi (Stendi) cha Shuleyatanga na Mfaranyaki kisha kuzungumza na madereva wa mabasi hayo ambayo yameenda sambamba na sikukuu ya Krismas na mwaka mpya wa 2022.


Morimori amesema katika ukaguzi huo wamekagua mabasi ya abiria yanayoenda safari ndefu ndani ya Mkoa na Nje ya Mkoa pamoja na daladala zinazofasafirisha abiria katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea .


Katika zoezi hilo wamekagua jumla ya magari 43 kati ya hayo magari 12 yamebainika kuwa ni mabovu ambayo yameondolewa barabarani hadi yatakapofanyiwa matengenezo na wamiliki wa magari hayo na kwamba madereva watatu wa daladala zilizokutwa kuwa ni mbovu wakati ukaguzi ukiwa unaendelea kwenye kituo cha daladala Mfaranyaki walikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Ruvuma Salum Morimori akizungumza na madereva wa vyombo vya moto.

Amefafanua kuwa katika ukaguzi huo makosa yaliyobainika kuwa ni ubovu wa taa,ubovu wa viti,msukani wa magari kutokuwa na nguvu na tatizo la kutokuwa na breki za uhakika jambo ambalo ni hatari kwa abiria pia dereva wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mmoja kubainika kuwa hana sifa (Deiwaka)na mwingine kukutwa akiwa amelewa pombe.


Morimori amesema kuwa ukaguzi huo utakuwa endelevu sio kwa sababu ya sikukuu pekee ,hivyo amewaonya kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria za usalama barabarani .


Naye ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya usafirishaji wa Nchi kavu (LATRA)Mkoani Ruvuma Sebastian Lohay amesema ofisi yake itaendelea kusimamia taratibu zote za usafirishaji ikiwemo na wanaokatisha Safari (ruti) walizopangiwa.

Baadhi ya madereva wa mabasi wakimsikiliza mkuu wa usalama barabarani Mkoani Ruvuma Salum Morimori ambaye hayupo pichani.

Mkuu wa usalama barabarani Mkoani Ruvuma Salum Morimori akiwa ndani ya basi kukagua usalama wa abiria.



Post a Comment

0 Comments