WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII DKT.NDUMBARO AVITEMBELEA VITUO VYA KULELEA WATOTO WA MAZINGIRA HATARISHI,SONGEA.


Waziri wa Maliasili na utalii ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro akimkabidhi zawadi mbalimbali kwenye kituo cha watoto wa mazingira hatarishi cha Mtakatifu Anthony anayepokea ni mtawa Judith Mwageni.

Na Amon Mtega,Songea.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Mkoani Ruvuma Dkt Damas Ndumbaro amewataka wakazi mbalimbali wa Jimbo hilo kujitolea kwenda kwenye vituo wanavyolelewa watoto waliochukuliwa katika mazingira hatarishi (Yatima) ili kubaini changamoto zao kisha kutoa misaada kwa watoto hao.

Dkt Ndumbaro ameutoa wito huo akiwa ametembelea vituo vitatu vya kulelea watoto hao ambavyo cha Mtakatifu Anthony kilichopo kata ya Mfaranyaki,Swacco kilichopo Mwengemshindo na Mtakatifu Tereza kilichopo Msamala kisha kutoa zawadi za sikukuu ya Krismasi na kuwatakia heri ya sikukuu hiyo pamoja na mwaka mpya wa 2022 .

Watoto wa kituo cha Mtakatifu Tereza wakiwa wamebeba zawadi ya Waziri wa Maliasili na utalii Dkt Damas Ndumbaro.

Waziri huyo akiwa ameambatana na Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Hamis Abdalah Ally pamoja na familia yake amesema kuwa kama jamii itajenga tabia ya kuwatembelea watoto wanaolelewa kwenye vituo hivyo basi changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto hao zingetatuliwa.

Dkt Ndumbaro ambaye ametoa zawadi mbalimbali kwenye vituo hivyo ambavyo ni Mchele,Unga, Sukari, mafuta ya kupikia vyakula na mafuta ya kupakaa Mwilini, Sabuni pamoja na vinywaji baridi(Juisi) amesema kuwa watoto waliopo kwenye vituo hivyo ni watoto wetu sote maana wengi wao ukifuatilia Historia yao hawawafahamu Wazazi wao zaidi ya sisi tunaoenda kuwapatia misaada.


Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo licha ya kutoa zawadi hizo lakini bado amewachukua watoto wanne kwenye vituo hivyo waliohitimu darasa la saba kwenda kuwasomesha katika shule za Sekondari za kulipia ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na walezi wa vituo hivyo.

Amefafanua kuwa baada ya kubaini changamoto zinazowakabili watoto hao aliamua kuanzisha mchezo wa gofu ambao uliwakusanya marafiki zake wengi kisha kumchangia fedha kwaajili ya kununulia zawadi kwa watoto hao.


Nao Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA) wakiwa wameambatana na Waziri huyo wamechangia magodoro huku kituo cha Swacco kikiwa kimepatiwa na vitanda sita vyenye mfumo wa mbili kwa moja ili kuboresha mazingira ya kulala watoto hao.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Songea Mjini Hamisi Abdalah Ally akimshukuru mmoja wa walezi wa watoto hao

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Hamisi Abdalah Ally amewapongeza wanaosimamia vituo hivyo kuwa na moyo wa upendo jambo ambalo jamii inatakiwa kujifunza kutoka kwa wasimamizi wa vituo hivyo.


Naye Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amesema kuwa Manispaa hiyo itaendelea kushirikiana na vituo vyote vya kulelea watoto vilivyopo kwenye Manispaa hiyo ili kubaini changamoto wanazokutana nazo.


Pia mmoja wa walezi wa watoto hao mtawa Judith Mwageni wa kituo cha Mtakatifu Anthony kilichopo Mfaranyaki amesema kuwa watoto hao huchukuliwa katika mazingira hatarishi hivyo changamoto za kuwatimizia mahitaji yao ni kubwa.

Waziri wa Maliasili na utalii ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro akiwa na familia yake akipokea zawadi ya keki iliyotolewa na watoto wa kituo cha Swacco ikiwa ni sehemu ya kutambua kazi zinafanywa na Waziri huyo.

Aidha watoto wa vituo hivyo ambavyo vimetembelewa na Waziri huyo wamemshukuru Waziri huyo kwa upendo wake ,huku watoto wa kituo cha Swacco wakitoa nao zawadi ya keki kwa Waziri huyo ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake kwao huku wakisema amekuwa akiwatembelea mara kwa mara.


Post a Comment

0 Comments