Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza jinsi miundombinu ya kwenye barabara inavyoharibiwa wakati wa kikao cha barabara mkoani humo. |
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge ametoa wito kwa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani humo kuungana na Halmashauri za mkoa huo kuunda sheria ndogondogo za matumizi ya barabara ili zisiharibiwe.
Wito huo ameutoa wakati akiongoza kikao cha bodi ya barabara pamoja na Wakala wa barabara za mijini na Vijijini (TARURA) kisha kujadili changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu unaofanywa na baadhi ya wakazi wa maeneo ambayo wamepitiwa na barabara hizo.
Ibuge akizungumza kwenye kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo na baadhi ya wabunge wa majimbo ya Mkoani humo amesema kumekuwepo na uharibifu wa miundombinu kwenye barabara hizo ikiwemo kwa baadhi ya magari makubwa ya mizigo (Malori) hasa yanayobeba makaa ya mawe humwaga au kupakia maeneo ya barabara jambo ambalo amesema halikubaliki kwa kuwa ni uharibifu.
Mkuu huyo amesema kuwa zikiwekwa sheria ndogondogo za kudhibiti uharibifu huo zitasaidia kupunguza uharibifu unaofanywa na baadhi ya watu hao ambao hawana nia njema.
Aidha mkuu huyo amesema kuwa mkoa wa Ruvuma unaenda kufungua barabara nyingi za Mijini na Vijijini hivyo miundombinu yake inatakiwa kuilinda kwa nguvu zote.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Songea mjini ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro amewataka watalaam wa barabara wakae kuangalia namna ya kuongeza bajeti kutokana na ukubwa wa eneo la mraba la mkoa huo ambalo linasikwea Kilomita 86,000, ikilinganishwa na bajeti inayotolewa havifanani.
Ndumbaro amesema kuwa mkoa huo hadi sasa hakuna barabara ya kiwango cha lami inayounganisha Nchi na Nchi hivyo barabara ambazo tayari zipo kwenye mpango wa kuunganisha Nchi na Nchi zifanyiwe kazi haraka ili mkoa huo uweze kufunguka na hatimaye Manispaa ya Songea ipewe hadhi ya kuwa Jiji.
Naye Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano ameitaka Tanroads mkoani humo kufanya upanuzi wa barabara ya Songea –Njombe kuanzia kata ya Mshangano hadi kwenye kituo cha mabasi (Stendi) iliyopo kata ya Shuleyatanga pamoja na kuweka taa za barabarani ili kupunguza ajali zinazotokana na msongamano.
Meneja wa Tanroads mhandisi Ephatar Mlavi akisikiliza kwa umakini hoja zinazotolewa na wajumbe wa kikao cha barabara mkoa wa Ruvuma. |
Meneja wa Tanroads Ruvuma mhandisi Ephatar Mlavi akipokea maagizo hayo amesema kuwa yataenda kufanyiwa kazi likiwemo la upanuzi wa barabara kutoka kata ya Mshangano hadi kata ya Shuleyatanga kwenye kituo cha mabasi .
0 Comments