WAZIRI wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Mkoani Ruvuma Dkt Damas Ndumbaro amewataka wakazi wa Jimbo hilo na maeneo mengine kuitumia Hifadhi ya Wanyamapori ya Ruhila (ZOO) kwa kufanyia shughuli za mikutano au sherehe ili kuitangaza hifadhi hiyo katika maeneo mbalimbali.
Dkt Ndumbaro ameutoa wito huo wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa jimbo hilo ambao walihudhuria sherehe za mwaka mpya wa 2022 katika eneo la hifadhi hiyo inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ipo ndani ya Manispaa ya Songea mkoani humo .
![]() |
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro akizungumza na moja ya Wananchi wake waliokuwepo kwenye sherehe za mwaka mpya wa 2022 zilizofanyika katika Hifadhi ya Ruhila. |
Waziri Dkt Ndumbaro akizungumza na wakazi hao ambao katika sherehe hiyo walipata kitoweo cha nyama pori (Nyati) amesema kuwa wakazi wa Jimbo hilo wana kila sababu ya kujivunia hifadhi hiyo kwa kuwa ipo mjini Songea jambo ambalo hata utalii wake hautumii gharama kubwa kufika katika eneo la hifadhi hiyo .
Licha ya kuwataka wakazi hao kuitangaza hifadhi hiyo kwa kwa kwenda kufanyia vikao mbalimbali pamoja na sherehe amesema kuwa Wizara imejipanga kupaboresha zaidi kwa kujenga uzio ambao umeshatengewa fedha Sh.Milioni mia tano (sh.500 milioni) ambazo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuboresha sekta ya utalii ili kuwavutia watalii wengi hapa Nchini.
Dkt Ndumbaro ambaye hadi sasa akiwa jimboni kwake ameshatembelea milima ya uhifadhi wa Misitu ya Matogoro kisha kuzungumza na mamia ya wakazi wa Jimbo hilo amesema kuwa katika mikakati ya kuboresha hifadhi hiyo ni pamoja na kuongeza Wanyama ambao wanadaiwa ni wakali kama Simba ,Chui ,Mamba na Twiga ili watalii wakifika katika eneo hilo wasikose kuwaona wanyama hao na kuwa ameshapatikana mwekezaji atakayejenga hoteli katika eneo hilo kwaajili ya wageni wa kutoka mikoa mbalimbali.
Aidha Waziri huyo akiwa katika hifadhi hiyo alipita kuzungukia baadhi ya maeneo ambayo yametengwa kwaajili ya uwekezaji wa vitu mbalimbali ambapo katika mizunguko hiyo ametumia usafiri wa Baiskeli .
![]() |
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini Hamisi Abdalah Ally akiwapongeza Wafanyakazi wa TAWA kwa kuilinda Hifadhi hiyo yenye miti asili . |
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Songea mjini Hamis Abdalah Ally amewapongeza wafanyakazi wa TAWA,kwa kazi kubwa wanayoifanya katika hifadhi hiyo hasa ya kuilinda miti ya asili (Pori) isivamiwe na watu ambao hawajui nini maana ya uhifadhi .
![]() |
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro kwa kuimarisha Hifadhi hapa Nchini. |
Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amempongeza Waziri Dkt Damas Ndumbaro kwa kutekeleza ilani ya CCM kikamilifu katika sekta ya Maliasili na Utalii jambo ambalo limefanya kuwaleta watalii wengi kwenye vivutio mbalimbali vya hapa Nchini.
0 Comments