Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro akiongoza mamia ya wakazi wa Jimbo hilo kuchukua kitoweo cha nyama pori(Nyati)ikiwa ni sehemu ya utoaji wa Elimu umuhimu wa kulinda rasilimali za Taifa.

Na Amon Mtega, Songea

WAZIRI wa Maliasili na Utalii ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Mkoani Ruvuma Dkt Damas Ndumbaro amewataka wakazi wa Jimbo hilo na mkoa mzima kwa ujumla kutumia vema vivutio vya utalii vilivyopo kwenye Mkoa kwa kufanya utalii ili waweze kutambua rasilimali zilizopo Mkoani humo.


Wito huo ameutoa wakati alipoongoza mamia ya wakazi wa Jimbo la Songea mjini kwenda kusherekea mwaka mpya wa 2022 kwa kufanya utalii wa ndani
katika hifadhi ya misitu ya milima Matogoro iliyopo kata ya Ndilimalitembo katika Manispaa ya Songea ambayo inahudumiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).


Dkt  Ndumbaro akiwa na mamia ya wakazi hao katika hifadhi ya misitu ya milima ya Matogoro amesema kuwa Wananchi wakijenga tabia ya kutembelea hifadhi zilizopo kwenye maeneo yao watapata Elimu tosha ya kuzitambua rasilimali zilizopo pamoja na kujenga ushirikiano wa kuzitunza.


Katika hatua nyingine Waziri Ndumbaro na Mbunge wa Jimbo la Songea mjini amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwemo kutoa fedha kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii za kukarabati miundombinu ya maeneo ya vivutio ili kuimarisha utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini akicheza ngoma (Lizombe) ikiwa ni sehemu ya kudumisha tamaduni za kingoni.

Amesema kuwa katika suala la miundombinu kwenye maeneo ya hifadhi ya milima Matogoro Waziri huyo amesema Wizara hiyo imejipanga kupitia fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kujenga barabara ya uhakika itakayofika hadi juu ya misitu ya milima Matogoro ili kuwarahisishia wanaoenda kufanya utalii.


Aidha Waziri Ndumbaro akiwa katika milima hiyo amewaonyesha wakazi wa Jimbo maana halisi ya Utalii kwa kuwagawia matunda ya porini yanayopatikana kwenye msitu huo yajulikanayo kwa jina la Masuku ambayo huliwa sana na wanyama wa aina mbalimbali hasa Nyani pamoja na binadamu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoani Ruvuma Oddo Mwisho akimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye Wizara yake.

Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoani Ruvuma Oddo Mwisho ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Waziri Dkt Damas Ndumbaro kuwa ni Wizara ambayo kwa sasa imejipanga kikamilifu katika kuleta mabadiliko makubwa kwenye suala la Utalii ndani ya Nchi yetu ya Tanzania.

Hata hivyo mwenyekiti Mwisho pia amewapongeza Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS)ambao wapo chini ya Wizara hiyo kwa kufanya kazi ya kuhudumia hifadhi ya milima Matogoro ambayo pia ni sehemu ya vyanzo vya maji ambayo yanayotumika katika Manispaa ya Songea na pia ndiyo chanzo cha mto mkubwa uitwao Ruvuma ambao ndio uliobeba jina la Mkoa wa Ruvuma.

Kamanda wa TFS kanda ya kusini Manyisye Mpokigwa akishukuru ushirikiano wanaoupata kutoka ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro.

Kwa upande wake Kamanda wa Wakala wa Misitu Tanzania TFS kanda ya kusini Manyisye Mpokigwa ameshukuru ushirikiano unaofanywa na ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii katika kuendelea kuimarisha vivutio pamoja na kuzilinda hifadhi ikiwemo ya Misitu.

Diwani wa kata ya Majengo Abdulqadir Hussen akiwa amesimama kwenye baadhi ya maeneo yenye vivutio katika milima ya Matogoro .

Naye diwani wa kata ya Majengo Manispaa ya Songea Abdulqadir Hussen amesema kuwa kilichofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii ni Elimu tosha kwa wakazi wa Jimbo la Songea kwa kuwa wengi wetu hatukujua kama milima ya Matogoro imekuwa na vivutio vizuri hivyo ikiwemo hali ya hewa iliyopo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Songea mjini akimpa matunda ya porini  (masuku )mmoja wa Wananchi wake wa Jimbo la Songea mjini Mohamed Mchele ikiwa ni sehemu ya kutambua matunda yanayotokana na misitu hiyo.

Katika utalii huo mamia hao wamepata fursa ya kupata kitoweo cha nyama ya pori (Nyati) bure kwa lengo la kutoa elimu kwa wakazi hao umuhimu kulinda rasilimali zilizopo ili vitoweo viendelee kupatikana hadi kwa vizazi vijavyo.