KIJANA mmoja mwenye umri kati ya miaka (30) na (40) mkazi wa Mtaa wa Vitendo kata ya Misugusugu Wilayani Kibaha (jina limehifadhiwa) anasakwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa tuhuma za kumbaka kisha kumuua mwanafunzi (7) wa darasa la pili.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo ACP Pius Lutumo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 30 mwaka huu huko mtaa wa Vitendo kata ya Misugusugu.
Lutumo amesema kuwa mtuhumiwa huyo ametoroka mara baada ya tukio hilo ambapo anatuhumiwa kumbaka na kumuua kwa kumziba na chandarua mdomoni ili asipige kelele.
Amesema mwanafunzi huyo wa darasa la pili mwenye umri wa miaka (7) alikuwa anasoma shule ya Msingi Misugusugu.
Aidha amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alifanya tukio hilo la mauaji wakati akimbaka mwanafunzi huyo ambapo alimziba mdomo kwa kutumia chandarua ili asipige kelele hivyo kusababisha kifo hicho.
Ameongeza kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwafuatilia watoto wao na kuzungumza nao mara kwa mara juu ya kujilinda wenyewe kwa kutoa taarifa za haraka juu ya wanaowasumbua.
0 Comments