Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dr.Julius Ningu akifungua maji ya kisima yaliyotolewa msaada na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. |
MKUU wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dr.Julius Ningu ameishukuru kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa ushirikiano mbalimbali wanaoufanya kwenye jamii katika suala zima la kuchangia na kutoa misaada kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye Wilaya hiyo.
Shukrani hizo amezitoa wakati akipokea msaada wa Gari aina ya Canter iliyosajili kwa namba SM,14226 yenye thamani ya Sh.Milioni 50 pamoja na kisima cha maji ya bomba chenye thamani ya Sh.Milioni 29 vyote vikiwa vimetolewa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayo jishughulisha na madini ya Uranium katika mto Mkuju uliopo kata ya Likuyuseka Wilayani humo.
Hilo ndilo Gari aina ya Canter uliyotolewa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwaajili ya matumizi ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. |
Dr.Ningu amesema kuwa msaada wa gari hilo na maji hayo vitatumika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ambayo inaendelea kuimarishwa miundombinu yake kwenye baadhi ya majengo yaliyopo Hospitalini hapo.
Mkuu huyo amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikichangia shughuli mbalimbali za kijamii katika suala zima la maendeleo hivyo amewataka na wadau wengine kuungamkono jitihada hizo ili kuiinua Wilaya hiyo kimaendeleo .
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited Frederick Kibodya akizungumzia kazi zinazofanywa na Kampuni hiyo |
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mantra Fredrick Kibodya awali wakati akisoma taarifa ya ufanyaji kazi amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa siku zote ikisaidiana na jamii katika nyanja za Afya,Elimu ,Usalama barabarani hasa kwa watoto wa shule ,Utunzaji wa Mazingira pamoja na Michezo.
Hata hivyo mkurugenzi Kibodya amepokea ombi lililoombwa na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa la msaada wa bati za kuezekea baadhi ya Nyumba zilizoezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali katika Kijiji cha Likuyuseka ,ambapo mkurugenzi huyo ameridhia kutoa Sh.Milioni 10 kwaajili ya ununuzi wa bati hizo.
Naye mbunge wa Jimbo hilo Vita Kawawa ameishukuru kampuni ya Mantra huku akiahidi kushirikiana nao bega kwa bega katika kuhakikisha mradi wa uchimbaji wa madini ya Uranium unaanza ili kupanua fursa kwa wakazi wa Wilaya hiyo kwa kuwa Wilaya hiyo haina hata kiwanda kimoja hivyo tegemeo kubwa ni mradi wa kampuni hiyo.
Pia mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya hiyo DR.Lucia Kafumu amesema kuwa msaada wa visima vya maji hayo pamoja na Gari hilo vitasaidia katika Hospitali hiyo ambapo awali kulikuwa na changamoto ya mahitaji hayo .
0 Comments