WAZIRI wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt,Damas Ndumbaro amewataka wakazi wa Jimbo hilo kutumia vema fursa mbalimbali zikiwemo za ajira dhidi ya wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza kwenye jimbo hilo.
Wito huo ameutoa wakati akizindua eneo la uwekezaji wa Viwanda lililopo kata ya Lilambo Manispaa ya Songea mkoani humo ambapo uzinduzi huo umeenda sambamba na kuvitambua vikundi kumi na moja (11) vya Ujasiliamali ambavyo vimepatiwa mkopo wa sh.Milioni 465 kwa makundi ya fani mbalimbali ikiwemo ya udizaina(ushonaji nguo).
Dkt.Ndumbaro akizungumza kwenye uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na watu mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo mwenyekiti wa wafanyabiashara wa China hapa Africa Xian Qsag(Komba)amesema kuwa kama wakazi wa Jimbo hilo watatumia ipasavyo fursa zinazoletwa na wawekezaji basi Manispaa hiyo itabadilika kwa kasi kiasi cha kuitwa jiji.
Mbunge huyo amesema kuwa eneo hilo walilotengewa wawekezaji wa Viwanda litatumika ipasavyo ikiwemo na kuweka miundombinu stahiki ili wajasiliamali ambao wengi wao wanaopatiwa mikopo ya asilimia kumi (10)za mapato ya ndani waweze kunufaika zaidi.
Baadhi ya vikundi vya wajasiliamali vikipokea hundi za mikopo wa pili kushoto ni mfanyakazi wa benki ya NMB ,Songea ,Juliana Tinda. |
Aidha Mbunge huyo wakati akikabidhi hundi za malipo kwenye vikundi hivyo ambapo fedha hizo zimewekwa kwenye akaunti za benki mbalimbali za mjini Songea ikiwemo ya NMB amesema kuwa sasa ni wakati mzuri wa kufanya kazi kwa kujituma zaidi.
Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kueleza mambo kadhaa hasa ya miradi iliyofanywa na jimbo hilo katika sekta mbalimbali kama ya Afya ,Elimu ,Barabara huku miradi miwili ya ujenzi wa Dampo na Soko la Mazese ambayo inadaiwa kunyang’anywa akifanikiwa kuirudisha.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Philipo Beno akizungumzia mikakati mbalimbali juu ya kuviimarisha vikundi vya wajasiriamali ili viweze kuwa na sifa ya kukopesheka. |
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Beno Philipo awali wakati akisoma taarifa amesema vikundi vilivyopatiwa mikopo hiyo ni Vijana ,Wanawake na Walemavu na kuwa walemavu wamekuwa warejeshaji wazuri wa mikopo hiyo.
Philipo amesema Halmashauri itaendelea kuvijengea uwezo vikundi pamoja na kutoa vifaa kwenye vikundi hivyo badala ya kuwapatia fedha ambazo baadhi yao wamekuwa wakigawana bila kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri hiyo pamoja na timu yake kuhakikisha wanakusanya fedha za madeni zilizopo kwenye vikundi vilivyokopa ili kutoa fursa kwa vikundi vingine viweze kukopeshwa.
Hata hivyo diwani wa kata ya Lilambo Yobo Mapunda amewaomba watalaamu wa mipangomiji kutoka manispaa kwenda kupima maeneo hayo haraka ili kutoa fursa ya wawekezaji kujenga.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa China hapa Africa Xian Qsag (Komba) ambaye ameonyesha nia ya kuwekeza kiwanda katika eneo hilo amesema kuwa Songea ni kati ya maeneo mazuri barani Africa kwa uwekezaji huku akiwaomba wakazi wa Jimbo la Songea kutambua jitihada zinazofanywa na mbunge wa Jimbo hilo za kuwapelekea maendeleo watu wake.
Mmoja wa waliopatiwa mikopo hiyo Josephina Mhagama ambaye ni mwenyekiti wa kikundi cha ufundi dizaina (Ushonajinguo) kilichopo Mjimwema ameipongeza Serikali pamoja na wakuu wa idara ya Manispaa ya Songea kwa kukitambua kikundi hicho kisha kupatiwa mkopo jambo litakalo wasaidia kuongeza ajira kwa vijana.
0 Comments